Halloween Costume ideas 2015
January 2016

Bondia wa zamani mbabe aliyeweka rekodi za nguvu kwenye mchezo wa ngumi, Mike Tyson ameamua tu kutuonesha kwamba kama huwezi kutembelea hoverboard, basi wewe achana nazo tuu hata usijaribu kucheza nazo.
Hii video aliipost Mike Tyson kwenye ukurasa wake Instagram ambapo kuna sauti ya mtoto wa kike inaonekana kama anamuonya hivi kwamba ataanguka, lakini Mike akaendelea zake.. sekunde chache mbele mambo yakaenda kombo !!
Ilikuwa stori yenye uzito wake kiasi cha kwamba TV ya CNN waliiripoti hii.

Chuo kikuu cha Garissa kilichofungwa mwaka uliopita baada ya watu 148 kuuawa kwenye shambulio lililotekelezwa na wanamgambo wa al-Shabab, kimefunguliwa tena.
Wafanyakazi wamefika kazini leo huku usalama ukiwa umeimarishwa.
Kila aliyekuwa akiingia katika chuo kikuu hicho kilichoko eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya amepekuliwa na maafisa wa usalama.
Kituo cha polisi, ambacho kitakuwa na maafisa zaidi ya 20 wa kutoa ulinzi, kimejengwa ndani ya chuo kikuu hicho.
Kitambulisha mada #GarissaUniversityReopens (Chuo Kikuu cha Garissa chafunguliwa tena) kimekuwa kikivuma katika mtandao wa Twitter nchini Kenya.
Wengi wanasema kufunguliwa kwa chuo hicho kunaonyesha Wakenya hawawezi kuvunjwa moyo na magaidi.
Msimamizi mkuu wa chuo kikuu hicho Prof Ahmed Warfa ameambia BBC kwamba wanafunzi wataanza kufika chuoni Jumatatu ijayo tarehe 11 Januari.
Hakukukuwa na sherehe yoyote maalum ya kuadhimisha kufunguliwa upya kwa chuo hicho.
Wengi wa wanafunzi wanaofadhiliwa na serikali walionusurika shambulio hilo la mwezi Aprili walihamishiwa Chuo KIkuu cha Moi, Eldoret.
Wanafunzi wa kujitegemea ndio wanaotarajiwa kurejelea masomo Jumatatu.
Mwandishi wa BBC Bashkas Jugsodaay anasema kufunguliwa kwa chuo kukuu cha Garissa ni afueni kwa wakazi na viongozi wa mkoa wa Kaskazini Mashariki ambao wamekuwa wakiisihi serikali kufungua chuo hicho, kwa walikuwa wakikitegemea kwa ajira na wateja. Wengi walikuwa wakinufaika
Wanafunzi zaidi ya 800 walikuwa wakisomea taaluma mbalimbali katika chuo hicho kabla ya kushambuliwa na magaidi Aprili mwaka jana.

Saudi Arabia imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya Iran na huku kukiwa na hali mbaya ya mvutano kufuatia utekelezaji adhabu ya kifo kwa mhubiri maarufu wa dini ya Kiislamu.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Saudia, Adel al-Jubeir, ameishutumu serikali ya Iran kwa kusambaza silaha na kuanzisha jela na kuwafunga watu wanaodhaniwa magaidi katika ukanda wake .
Waziri huyo amesema wanadiplomasia wa Iran wanatakiwa kuondoka Saudia ndani ya saa arobaini.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, waandamanaji mjini Tehran waliuvamia ubalozi wa Saudia mjini Tehran, huku wakilaani utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa Sheikh Nimr al-Nimr na watu wengine 46.
Watu hao waliouawa inasadikiwa walikuwa na hatia ya makosa yanayohusiana na ugaidi.
Kiongozi mkuu wa Iran alimweleza Sheikh huyo kama shahidi ambaye alikuwa akitetea amani na kufanya maandamano ya amani.

NICKSON JOHN

Staa wa R&B wa Marekani Chris Brown amekuwa haishiwi headlines..baada ya matukio mfululizo yakimuhusisha na Polisi, headlines zimerudi tena kwake.
Ukiachia lile tukio la kumpiga mwanamuziki mwenzake Rihanna mwaka 2009 na kutakiwa kutojihusisha na kosa lolote kwa miaka mitano hili ni tukio lingine lilolomrudisha kwenye mikono ya polisi huko Las Vegas.
Jana jumamosi akiwa katika klabu ya The Palms Casino Resort staa huyo anadaiwa kumpiga usoni mama mmoja Liziane Gutierrez ambaye alikua akijaribu kumpiga picha.
Liziane Gutierrez
Polisi katika jiji la Las Vegas, Marekani bado wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na malalamiko ya mama huyo
Mwaka 2009, Brown aliagizwa kukaa miaka mitano bila kufanya kosa baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga nyota wa muziki wa pop Rihanna.

Mashabiki wengi  wa soka wanaamini nyota wa Real Madrid Cristiano Ronaldo ndiye bora duniani..lakini kuna hili gazeti moja kutoka Ufaransa la L’Equipe limeorodhesha wachezaji 100 waliofanya vizuri kwa mwaka uliopita wa 2015.
Katika orodha hiyo Ronaldo pamoja na mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski wamefanikiwa kuingia hatua ya tano bora.
Mastaa waliofanikiwa kushika nafasi tatu za juu ni Lionel Mess, Neymar pamoja na Luis Suarez.

Pathankot
Maofisa wa polisi wakiweka doria nje ya kambi hiyo baada ya  uvamizi.



Washambuliaji wanne wameuawa baada ya wanajeshi wa India kuzima shambulio la mapema asubuhi katika kambi la jeshi la wanahewa karibu na mpaka wake na Pakistan.
Wanajeshi wawili wa kambi hiyo ya Pathankot pia waliuawa kwenye makabiliano na wapiganaji hao, ambayo yalidumu saa kadha.

Kambi hiyo imo kwenye barabara kuu ya kuelekea sehemu ya Kashmir inayodhibitiwa na Kashmir.
Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya viongozi wa India na Pakistan Narendra Modi na Nawaz Sharif kukutana mjini Lahore kuzindua mpango wa ghafla wa kutafuta Amani.
Jimbo lote la Punjab nchini India limewekwa katika hali la tahadhari.
Watu hao walioshambulia kambi hiyo wanadaiwa kuvalia sare za jeshi la India na walitumia gari walilokuwa wameteka nyara.

Waliingia maeneo ya makazi ya wanajeshi kambini lakini wakakabiliwa vikali na hawakuweza kuharibu vifaa vya jeshi, msemaji wa jeshi la wanahewa Rochelle D'Silva amesema.
Mwandishi wa BBC Sanjoy Majumder akiwa Delhi anasema bado haijabainika washambuliaji hao walikuwa kina nani lakini wanashukiwa kutoka kundi la wapiganaji wa Kashmir kutoka upande unaodhibitiwa na Pakistan.

Hata hivyo, shirika la habari la AFP limemnukuu afisa mmoja wa usalama akisema wanaaminika kuwa wa kutoka kundi la Jaish-e-Mohammed.

India inamini kundi hilo husaidiwa na Pakistan, madai ambayo taifa hilo limekanusha.
Mwezi Agosti, watu saba waliuawa katika shambulio sawa, watu wenye silaha waliposhambulia kituo cha polisi wilaya ya Gurdaspur.

Jumapili
Majeshi ya serikali yalipoukomboa mji wa Ramad siku ya jumapili



Wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS) wameshambulia kambi ya jeshi karibu na mji wa Ramadi, siku chache baada ya mji huo kukombolewa na wanajeshi wa serikali.

Msemaji wa jeshi amesema washambuliaji waliokuwa kwenye ndege lililotegwa mabomu na wengine waliovalia mikanda ya kujilipua walishiriki shambulio hilo.

Jeshi lilikabiliana nao likisaidiwa kutoka angani na majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani.
Serikali ya Iraq ilitangaza kwamba ilikuwa imefanikiwa kuukomboa mji wa Ramadi kutoka kwa IS Jumapili.

Wapiganaji hao walikuwa wameushikilia mji huo mkubwa tangu Mei.
Shambulio la Ijumaa ndilo la karibuni zaidi kutekelezwa na IS dhidi ya wanajeshi wa Iraq tangu kukombolewa kwa Ramadi.
Mtathmini wa BBC anayeangazia masuala ya Mashariki ya Kati Sebastian Usher, anasema shambulio hilo linaonyesha kibarua ambacho majeshi ya serikali yanakabiliwa nacho kulinda mji wa Ramadi.

 Kiwanda

Waislamu 200 wanaofanya kazi katika kiwanda kimoja cha nyama Colorado, Marekani wamefutwa kazi baada yao kugoma...,

 

Walikuwa wamegoma kulalamikia kunyimwa uhuru wa kuswali wakiwa kazini.
Wengi wao ni wahamiaji kutoka Somalia.
Msemaji wa Baraza la Uhusiano wa Wamarekani na Waislamu Jaylani Hussein anasema wafanyakazi hao katika kiwanda cha Cargill Meat Solutions walikuwa kwa muda mrefu wameruhusiwa kuswali.
Msemaji wa kiwanda hicho cha Cargill alisema kuna uhuru wa kuabudu kiwandani lakini lazima mahitaji ya kuabudu yaambatane na mahitaji ya kazi kiwandani.

Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Haki za Kibinadamu Somalia Omar Jamal, amesema mameneja wanafaa kufahamu kwamba Waislamu huhitajika kuswali mara kadha kwa siku, hili likitegemea kipindi cha mwaka.

 


 
Familia nchini Uchina sasa zimeruhusiwa kupata watoto wawili baada ya kuanza kutekelezwa kwa sera mpya kuhusu upangaji uzazi.

Sera hiyo mpya imeanza kutekelezwa Ijumaa na kufikisha kikomo sera tata ya awali ambayo iliwaruhusu wanandoa kupata mtoto mmoja pekee.
Sera hiyo imesababisha kuwepo kwa sehemu kubwa ya raia ambao ni wazee na kupungua kwa watu ambao wanaweza kufanya kazi.

Sera hiyo ya watoto waili ilitangazwa Oktoba na chama tawala cha Kikomunisti na kuidhinishwa na bunge la taifa baadaye Desemba.

"Ni vyema kuzingatia jinsi maisha yataathirika,” shirika la habari la serikali la Xinhua limesema.
Sera ya kuruhusu mtoto mmoja pekee katika familia ilianza kutekelezwa mwaka 1978
Waliopata watoto zaidi waliadhibiwa vikali na hata wengine kulazimishwa kutoa mimba.
Sera hiyo ilizuia kuzaliwa kwa watu 400 milioni.
Wanandoa waliojifungua mtoto zaidi ya mmoja waliadhibiwa

Idadi ya watu Uchina kufikia 2013 wakati wa kufanywa kwa sensa ilikuwa imefikia 1.357 bilioni.
Kufikia 2050, Uchina inatarajiwa kuwa na watu karibu 500 milioni waliozidi umri wa miaka 60, idadi inayozidi raia wa Marekani.

Utafiti uliofanywa majuzi unaonyesha kwamba licha ya serikali kulegeza sheria ya kujifungua watoto, hakuna msisimko miongoni mwa wanandoa 100 milioni ambao wanaweza kupata watoto wa ziada.
Hii sana inatokana na gharama ya kuwalea watoto.

 

 

Klabu za Ligi Kuu ya England zitashuka dimbani kusaka alama za kwanza Mwaka Mpya leo Jumamosi, Arsenal wakijaribu kuendeleza uongozi kileleni kwa mechi ya nyumbani dhidi ya Newcastle.

Manchester United nao watakuwa nyumbani Old Trafford kusakata gozi dhidi ya Swansea ambao kwenye mechi za hivi karibuni wamekuwa wakiwalemea.

 

Manchester City watakuwa ugenini baadaye dhidi ya Watford. 


Chelsea watasubiri hadi Jumapili kujaribu bahati watakapokuwa ugenini dhidi ya Crystal Palace.

Ratiba kamili ya mechi ni kama ifuatavyo:
Jumamosi 2 Januari 2016 (Saa za Afrika Mashariki)
  • West Ham v Liverpool 15:45
  • Arsenal v Newcastle 18:00
  • Leicester v Bournemouth 18:00
  • Man Utd v Swansea 18:00
  • Norwich v Southampton 18:00
  • Sunderland v Aston Villa 18:00
  • West Brom v Stoke 18:00
  • Watford v Man City 20:30
Jumapili 2 Januari 2016
  • Crystal Palace v Chelsea 16:30
  • Everton v Tottenham 19:00
Jumanne 2 Januari 2016
  • Aston Villa v Crystal Palace 22:45
  • Bournemouth v West Ham 22:45

 

Makabiliano makali katika mkesha wa Mwaka Mpya baina ya wafungwa katika gereza moja la mashariki mwa Guatemala yamesababisha vifo vya watu wanane na wengine 24 kujeruhiwa. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, wawili kati ya waliokufa walikatwakatwa na kisha miili yao ikachomwa moto...,


 

 Polisi wa kutuliza ghasia walichukua udhibiti wa gereza hilo jana Ijumaa. Maafisa waligundua kuwa wafungwa hao walijaribu kutoroka kwa kubomoa ukuta wa gereza hilo la Puerto Barrios ambalo lina msongamano mkubwa kabisa wa wafungwa.

 Limejengwa kuwa na uwezo wa kuwahifadhi wafungwa 175, lakini sasa lina wafungwa 944. Tukio hilo ni la karibuni katika msururu wa mapigano ya gerezani nchini humo katika miaka ya karibuni. Mwezi Novemba mwaka jana, wafungwa 16 waliuawa kufuatia rabsha gerezani, huku wahanga watatu wakikatwakatwa vibaya.

Ulinzi katika kituo cha treni jijini Munich



Uchunguzi uliofanywa na vyombo vya habari vya Ujerumani umeonyesha kuwa maafisa walijua kuhusu uwezekano wa kutokea shambulizi katika mji wa kusini wa Munich kabla ya siku kuu ya Krismasi. 

Gazeti la Ujerumani la Süddeutsche, pamoja na mashirika ya utangazaji ya WDR na NDR yaligundua kuwa maafisa - wakiwemo wa ofisi za mambo ya ndani na mwendesha mashtaka - walikuwa na habari ya uwezekano wa kutokea shambulizi la kigaidi mjini Munich tangu Desemba 23. 

Mkuu wa polisi mjini Munich amesema walikuwa na "habari za kuaminika" kuhusu kitisho cha ugaidi, hali iliyowalazimu mamlaka mjini humo kufunga kituo cha treni. Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere amesema katika taarifa kuwa hali barani Ulaya na Ujerumani inaendelea kuwa mbaya katika Mwaka Mpya.


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametoa siku 30 kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), Dk Primus Nkwera kufanya ukaguzi wa vyuo vyote na kumkabidhi ripoti ili kujiridhisha na ubora wa elimu inayotolewa...,

Pia, amewataka watendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuandaa mitalaa yenye matokeo ya kujenga wanafunzi watakaozalisha kwenye jamii.

Waziri huyo ambaye amewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), alitoa maagizo hayo jana wakati wa ziara yake katika ofisi hizo ikiwa ni siku tano baada ya kuapishwa kuiongoza wizara hiyo.

Alisema anawafahamu vyema watendaji wote wa taasisi hizo na hatavumilia kuona ubora wa elimu ukiendelea kuporomoka nchini.

Aliitaka TET kuhakikisha mtalaa wa KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) kwa darasa la kwanza na la pili unapelekwa shuleni kabla ya Januari 13.

“Lakini pili, ningependa muanze kutumia walimu wastaafu kwenye uandaaji mitalaa hiyo na ukaguzi uimarike kwa wanafunzi, mnaweza kuwa na mitalaa mizuri lakini ufuatiliaji ukikosekana haitasaidia,” alisema.

Kuhusu ubora wa elimu alisema: “Ningependa uonekane kwa matokeo baada ya kumaliza shule, sihitaji kusikia amefaulu kwa alama ngapi ila amejengewa uwezo gani kichwani,” alisema.

Alisema kasi ya uwajibikaji TET imekuwa ndogo kwani kitabu cha kurasa 16 kinatengenezwa kwa mwaka mmoja. 

“Ninaweza kuja hapa mnipatie nafasi halafu tujipime na nyie tuone, naomba mbadilike nimeona mko nyuma sana ya kasi yangu,” alisema.

Mbali na maagizo hayo, Profesa Ndalichako aliiagiza Nacte kufanya usajili wa vyuo kwa kuzingatia mahitaji ya soko badala ya kusajili holela bila ufuatiliaji kwa kuwa baadhi vinajiendesha kwa ujanja ujanja.

Alisema suala la ubora wa elimu linamkosesha usingizi. Alilitaka baraza hilo kungeongeza kasi ya ushawishi katika uwekezaji wa shule za ufundi badala ya kujikita kwenye upandishaji wa hadhi ya vyuo na kuondoa dhana ya biashara katika sekta ya elimu.

“Lakini pia ningependa wafanyakazi wote mbadilike, tuache kufanya kazi kwa mazoea. Katika upandishaji hadhi ya vyuo, lazima tujiridhishe na mahitaji ya Taifa, pia kwa suala la udahili wa wanafunzi, ningependa vyuo ambavyo havijatambuliwa kwenye mfumo wa Necta viingizwe ili kuondoa udanganyifu wa vyeti wa usajili,” alisema.


Wakati operesheni ya kuweka alama ya X kwenye nyumba zilizojengwa mabondeni, maeneo ya wazi na kinyume na taratibu ikiendelea, Hoteli za Double Tree na Slip Way nazo zimekumbwa na pigo hilo.

Hoteli hizo pamoja na nyumba ya Maheshbhai Patel na baadhi ya wamiliki wengine wa nyumba ambao kuta zake zimejengwa karibu na barabara ya Slip Way eneo la Msasani Peninsula, wamepewa siku saba kuzibomoa.

Jana, uongozi wa Manispaa ya Kinondoni uliweka alama za X na kuwaonya wamiliki hao kwamba, wasipobomoa manispaa itazibomoa na kudai gharama za ubomoaji.

Akizungumza kwa simu jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema Serikali haitaurudi nyuma katika kutekeleza sheria hata kama kuna watu wana jeuri ya pesa.

Alisema Manispaa ya Kinondoni iliwapatia vibali vya kupendezesha maeneo ya pembezoni mwa barabara ikiwamo kupanda maua, lakini wao badala ya kutimiza masharti ya vibali walizungushia kuta jambo ambalo hawatalivumilia.

“Wangependezesha na kufunga minyonyoro kuzuia kuharibiwa mazingira yao kama walihisi wananchi wangeharibu, lakini siyo kujenga kuta.

“Nimewaagiza Kinondoni wawapatie notisi ya siku saba kubomoa kwa hiari. Wasisubiri Serikali ivunje.

"Tutabomoa hadi lile jengo lililopo karibu na Hospitali ya Ami lililovunja sheria, yule hawezi kuonyesha jeuri ya fedha,” alisema Lukuvi.

Alisema Serikali ina mpango maalumu wa kubomoa majengo yote yaliyojengwa kinyume na sheria Masaki na Oysterbay na wameanza na Barabara ya Slip Way.

Katika hatua nyingine, sakata la bomoabomoa pia limewakumba waliojenga katika hifadhi za mikoko baada ya watumishi wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na maofisa misitu wa Manispaa ya Kinondoni kuweka alama ‘X’ katika nyumba zaidi ya 30 ikiwamo ya kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God, Dk Getrude Rwakatare.

Kazi hiyo ilianza jana mchana katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ikiwamo, katika Mtaa wa Ally Sykes, Kawe na Jangwani Beach eneo la Mbezi Beach. Ofisa Misitu Msaidizi wa Manispaa ya Kinondoni, Issa Juma aliwaambia wanahabari kuwa kazi hiyo ni endelevu.
Jumba  la  Mchungaji Mama  Rwakatare
Jumba  la  Mchungaji Mama  Rwakatare


 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence S.Milanzi akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Jaji Meja Jenerali Projest A.Rwegasira akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais,Utumishi na Utawala Bora,Dkt.Laurian Ndumbaro akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Waandishi mbalimbali wa Vyombo vya Habari wakifuatilia kwa umakini hafla ya kuwaapisha kwa Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,Amina H.Shaban akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje,Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa,Balozi Ramadhan  Muombwa Mwinyi akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Immaculate Peter Ngwale akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wake iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi,Profesa Simon S.Msanjila akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wake iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,Profesa James Epifani Mdoe akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,James Dotto akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria,Amon Mpanju akila kiapo cha utii mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wake iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Makatibu Wakuu na manaibu wao kabla ya kuapishwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Pichani kuliani ni Makamau wa Rais Mh.Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa wakati wa hafla fupi ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao Ikulu jijini Dar,wa tatu kulia ni Mke wa Rais,Mama Janeth Magufuli pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Bwa.George Masaju.
Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa amembatana na  Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue wakiwasili kwenye hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu wao iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget