VIJANA GEUZENI CHANGAMOTO KUWA FURSA..,
Diana Isaya akipokea cheti kutoka kwa Meneja wa huduma kwa jamii, Hawa Bayumi baada ya kuhudhuria mafunzo ya ujasiriamali yaliyoendeshwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, Dar Live Dar es Salaam. Kulia ni Meneja mauzo wa Airtel, Fadhili Mwasyebya na mkufunzi wa mafunzo hayo Allen Mwangwele. |
VIJANA wametakiwa kuzigeuza changamoto zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuzifanya kuwa fursa kwao na kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa na kubaki wakilalamika kuwa hakuna ajira...,
Pamoja na fursa hizo vijana pia wametakiwa kuitumia mitandao ya kijamii kutengeneza mifumo ya kibiashara kwa kubadilishana mawazo badala ya kutumia muda mwingi mitandaoni kujadili mambo yasiyo na tija.
Rai hiyo ilitolewa jana na Meneja wa Huduma za Kijamii wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, Hawa Bayumi katika semina ya Airtel Fursa Tunakuwezesha inayotolewa Dar es Salaam kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 24 ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Alisema lengo la semina ni kuwapatia vijana waishio Dar es Salaam mafunzo ya biashara ya ujasiriamali kuweza kumudu uendeshaji biashara zao na mahitaji yao. Bayumi alisema: “Tumeamua kulenga kundi la vijana hawa kutokana na nguvu ya kundi hilo ambalo linauwezo wa kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi iwapo litawezeshwa kupata elimu ya ujasiriamali”.
Mmoja wa wanufaika mjasiriamali Diana Isaya alisema kuwa amepata muongozo mzuri utakaokuza biashara zake na kuzifanya kwa weledi mkubwa zaidi. “Napenda kuwahimiza vijana wenzangu kuandaa mawazo ya biashara bila kusubiri kuwa na fedha ndiyo waanze kujipanga na kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao,” alisema Isaya.
Tangu kuanza kwa mafunzo hayo ya ujasiriamali kwa vijana, zaidi ya mikoa 10 imefikiwa ambapo vijana wengi wamenufaika na mpango huo na kuanzisha ama kuendeleza biashara zao.