Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Ndugu Reverien Ndikuriyo Spika wa Seneti na Mjumbe Maalum wa Rais wa Burundi |
RAIS John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Seneti na Mjumbe Maalumu wa Rais wa Burundi, Reverien Ndikuriyo Ikulu jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini Burundi na jitihada zinazochukuliwa na Tanzania, ikiwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akiwasilisha ujumbe wa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kuhusu hali ya Burundi, Spika Ndikuriyo alisema Serikali ya Burundi ipo tayari kufanya mazungumzo na wadau wote wa siasa kuhusu hali ya nchi hiyo na jitihada za kuumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.
Akitoa maelezo ya kikao hicho kwa niaba ya Dk Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga alisema Serikali ya Burundi imekubali usuluhishi, unaofanywa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa niaba ya Marais wa EAC kutokana na kikao kilichofanyika Dar es Salaam Julai mwaka huu na kwamba Serikali ya Burundi iko tayari kushiriki mazungumzo hayo ya amani.
“Nimeagizwa nipeleke taarifa kwa mawaziri wa nchi za nje wa nchi jirani juu ya maandalizi ya mazungumzo hayo ambayo yataanza kule Uganda tarehe 28 mwezi Desemba”, alisema
Post a Comment