Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (Katikati) akizungumza na Mchezaji wa TP MAzembe Mbwana Samatta (Kushoto) alipotembelea ofisini kwake jana. |
DAR ES SALAAM
SERIKALI imempongeza mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta kwa juhudi alizoonesha katika kuisaidia timu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutwaa ubingwa wa Afrika, akihimiza Watanzania kumuunga mkono...,
Samatta jana alikwenda ofisini kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye kumuaga tayari kwa safari yake kuelekea Nigeria katika utoaji wa tunzo za wachezaji bora, akiwa ni miongoni mwa wanaowania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Nape alisema serikali ipo bega kwa bega na Samatta pamoja na wanamichezo wote, huku akimtakia kila la heri mchezaji huyo katika kinyang’anyiro hicho.
Alisema serikali inapambana ili kuhakikisha wanamichezo wote wanafaidika kutokana na kazi zao na itapambana na wale wote ambao wamekuwa wakila kupitia jasho la wanamichezo.
“Kwa niaba ya serikali, nakupongeza kwa hatua uliofikia, kwani hadi hapo umelitangaza vyema taifa letu, lakini pia hata tuzo ambayo unawania endapo utaitwaa itazidi kukutangaza wewe na pia nchi yetu,” Nape alisema serikali sasa inasimamia vyema maslahi ya wanamichezo wote ili wafaidike na kile ambacho wanakitolea jasho na kwamba lengo ni kuifanya michezo kuwa shughuli rasmi itakayonufaisha wachezaji na taifa.
Naye, Samatta alisema anatambua umuhimu wa mchango wa serikali katika kuchangia mafanikio yake pamoja na soka la Tanzania kwa ujumla na kuongeza kuwa, endapo atafanikiwa kutwaa tuzo hiyo basi haitakuwa ya kwake binafsi bali ni ya taifa zima.
“Kama nitafanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika tuzo hiyo haitakuwa ya kwangu peke yangu bali itakuwa ni ya watanzania wote,” alisema.
Alisema, “Kabla ya kwenda sehemu yoyote ile ni lazima upate baraka za wazee ndiyo maana nimekuja hapa kuaga na kuchota baraka za serikali kwa niaba ya Wizara inayohusika na michezo, kabla ya kuelekea Nigeria kuwania tuzo ya mchezaji bora Afrika.”
Samatta pia alimpongeza Nape kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge pamoja na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Tuzo za wachezaji bora Afrika zitatolewa nchini Nigeria Januari 7, 2016 ambapo Samatta anawania tuzo hiyo ya mcheaji bora Afrika kwa wachezaji wa ligi za Afrika akiwa pamoja na Bahgdad Bounejah (Etoile du Sahel, Tunisia) Algeria na Robert Kidiaba (TP Mazembe, Congo DR).
Post a Comment