Kiongozi wa wanamgambo wanaopigana nchini Yemen, Ahmed al-Idrisi, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akiwa safarini na wenzake wengine wanne maeneo ya kusini mwa mji wa Aden...,
Washambuliaji waliokuwa ndani ya gari na wengine juu ya Vifaru waliufyatulia risasi msafara huo na kumuua Ahmed al-Idrisi, kamanda wa ngazi ya juu wa kundi la upinzani linalounga mkono upande wa serikali,
Wakati wakiwa safarini katika barabara kuu ya wilaya ya Mansoura siku ya Jumatano.
Tukio hilo limekuja siku chache baada ya kuuliwa kwa hakimu maarufu katika barabara hiyo hiyo. Kwa mujibu wa madaktari, Hakimu muandamizi wa mji wa Aden, Jalal Abdullah, aliuliwa katika wilaya ya Mansoura Jumanne, masaa machache baada ya bomu kulipuliwa karibu na makao makuu ya chama cha Islah Islamist, na kujeruhi mtu mwingine mmoja. Hali hii imesababisha machafuko ya usalama katika mji ambao ndio makao makuu ya muda ya serikali ya nchi hiyo. Hadi sasa hakuna aliyejitokeza kuhusika na mashambulizi hayo.
Mashambulizi yakiendelea katika mji wa Aden, |
Katika miezi ya karibuni, mji wa kusini wa Aden umekuwa ukishuhudia msururu wa mashambulizi yanayowalenga wale wanaomuunga mkono Rais Abd-Rabu Mansour Hadi, ambaye serikali yake ina makao yake makuu mjini humo.
Wanamgambo wa kundi la Idrisi ni washirika wakuu wa muungano wa nchi za kiarabu ambao umekuwa ukilishambulia kwa mabomu kundi la waasi la Houthi linaungwa mkono na Iran, na lenye ngome yake katika mji wa Sanaa, kaskazini mwa Yemen.
Ushirikiano huwo uliingilia kati vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe tarehe 26 Machi na kuiunga mkono serikali ya rais Hadi.
Halikadhalika katika mji mwengine wa Taiz madaktari wameandamana baada ya hospitali moja kukataa kupokea wagonjwa wa ziada kutokana na kuwa na uhaba wa dawa, huku mapigano yakiwa yanaendelea mjini humo baina ya waasi wa Kihouthi na wanamgambo wanaunga mkono upande wa serikali.
Takriban watu 6,000 wameshauawa kutokana na mgogoro huwo na ingawa wanamgambo wa kusini mwa Yemen pamoja na vikosi vya muungano wa nchi za kiarabu waliwaondoa Wahouthi nje ya mji wa Aden Julai na kumuwezesha Rais Hadi kurudi tena, mapigano bado yamekuwa yakiendelea huku suluhisho la kidemokrasia likiwa bado halijapatikana.
Post a Comment