Dewji alitangaza kwenye chombo kimoja cha habari kuwa siku ya leo itakuwa ni mwisho akiutaka uongozi wa Simba kutoa majibu, kama yeye aweza kufanya uwekezaji huo na kuanza mara moja utekelezaji wa mikakati yake kuanzia Januari mwakani.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari juzi, msemaji wa Simba, Haji Manara alisema uongozi wa klabu hiyo haupingi uendeshaji wa klabu katika mfumo wa kisasa isipokuwa wanahitaji kuwa makini.
“Hakuna taasisi, mtu, kikundi aliyeleta barua kutaka kuinunua Simba mpaka hivi sasa, hatuna. Ni suala ambalo wanachama wanahitaji kuelimishwa kwanza kabla ya kuingia huko,”alisema.
Kwa mujibu wa taarifa za Dewji, anataka kuwekeza katika klabu hiyo kwa nia ya kuiendesha kibiashara.
Alisema alikutana na viongozi wa Simba, Rais Evans Aveva akiwa na Kassim Dewji na Musley Ruhwehi na kuwaeleza dhamira yake lakini anaona viongozi hao hawako tayari.
Pia, alisema iwapo ataruhusiwa kufanya uwekezaji huo atajenga kiwanja cha Bunju na kuwa kiwanja maalum cha mazoezi ya klabu hiyo na pia kama kituo maalum cha kulea vipaji vya soka kwa vijana ambao baadaye watachezea timu hiyo.
Dewji alisema iwapo leo halitatoka jibu kuwa uwekezaji huo ataachana nao na kuendelea na shughuli zake.
Hata hivyo, Rais wa Simba Aveva hivi karibuni alisema suala hilo haliwezi kuamuliwa haraka, kuna mchakato wa kupitia katiba na kufanyia marekebisho lakini pia kuwahusisha wanachama kwenye mkutano mkuu kisha waridhie ndipo jibu liweze kutoka.
Post a Comment